Monday, May 18, 2020

MBELGIJI WA YANGA AANZA MAMBO YAKE KWA KISHINDO!!!!!!!!!!!!


MICHAEL Sarpong, mshambuliaji wa zamani wa Rayon Sports ya Rwanda, ambaye hivi sasa ni huru anatua kuichezea Yanga katika kuelekea msimu ujao.

Mshambuliaji huyo raia wa Ghana, hivi karibuni mkataba wake ulivunjwa na Rayon kwa kile kilichoelezwa kuongoza mgomo wa wachezaji wakidai malipo ya mshahara wa mwezi Machi, mwaka huu.
  
Kwa mujibu wa Kocha Mkuu wa Yanga, Mbelgiji, Luc Eymael, mshambuliaji huyo ana sifa zote ambazo anazozitaka yeye, hivyo ana nafasi kubwa ya kutua kujiunga na Yanga katika msimu ujao.

Eymael aliitaja moja ya sifa hizo ni ujasiri aliokuwa nao wa kupambana bila ya kuwaogopa mabeki watukutu na watemi wa timu pinzani, jambo ambalo linamfanya aamini kuwa ni mtu sahihi kwenye timu hiyo.
  
“Sarpong yupo kwenye mipango yangu ya usajili katika msimu ujao, ninaamini viongozi hawatashindwana naye kwani ni mchezaji huru hivi sasa na uzuri tayari nimeanza mazungumzo na meneja wake.

“Na kama mazungumzo yakienda vizuri, basi atakuja Yanga kwani ni kati ya washambuliaji wenye sifa zote ambazo mimi ninazihitaji awe nazo mshambuliaji.

“Nimekuwa nikimfuatilia kwa karibu, hivyo ninamjua vizuri sina hofu ya uwezo wake, ninafanya mawasiliano na meneja wake kila kitu kinakwenda vizuri,” amesema Eymael.

NDEMLA BADO YUPO SANA SIMBA


IMEELEZWA kuwa Said Ndemla ameongezewa mkataba wa miaka miwili wa kuendelea kukipiga kwenye klabu hiyo kwenye msimu ujao baada ya kufikia muafaka mzuri na mabosi wake.


Awali, kiungo huyo alikuwa anatajwa kutimkia Yanga ambayo ilikuwa inatajwa kuwania saini yake kwa ajili ya kuiimarisha safu ya kiungo ya timu hiyo.

Mtoa taarifa huyo alisema kuwa, kiungo huyo amebakishwa kutokana na nidhamu kubwa aliyoionyesha akiwa na timu hiyo licha ya kutokuwepo katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo kinachonolewa na Mbelgiji, Sven Vandenbroeck.

Aliongeza kuwa kingine kilichombakisha ni uwepo wa viungo wakabaji wachache katika timu hiyo, licha ya kuwepo mipango ya kushusha kiungo mwingine mkabaji wa kimataifa mwenye uwezo mkubwa zaidi yake.

“Viongozi wamekubaliana kuwabakisha wachezaji wao waliowalea tangu wakiwa wadogo U20 kwa lengo la kutoondoka ndani ya kikosi hicho kutokana na uvumilivu waliokuwa nao wa kutoihama timu hiyo ambao ni Ndemla na Mkude (Jonas).

“Hivyo viongozi wamekubaliana kumbakisha, lakini amebakishwa kwa makubaliano ya kupambana katika timu ili apate nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo.

“Ndemla amekubaliana na hayo yote waliyokubaliana nayo huku akiomba mkataba wake uwe wa wazi utakaomruhusu kuondoka muda wowote kama akipata timu nje ya nchi,” alisema mtoa taarifa huyo.

Mtendaji Mkuu wa Simba, Senzo Mazingisa hivi karibuni aliwahi kuliambia Championi kuwa: “Kama uongozi tumepanga kuwabakisha wachezaji wote ambao mikataba yao inamalizika mwishoni mwa msimu huu kwa gharama yoyote lengo ni kuhakikisha tunasuka kikosi imara kitakachofanya vizuri katika msimu ujao.”

SIMBA KUPOTEZA MASTAA WAKE

SIMBA ipo nafasi ya kwanza kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara na pointi zake 71 kibindoni kuna mastaa ambao maisha yao yanafika ukingoni mwishoni mwa msimu ligi ikikamilika.

Ikiwa hawatamalizana na mabosi wao Simba kwa sasa basi itakuwa njia nyeupe kwao kusepa timu nyingine bure kabisa.

Mastaa hao ni pamoja na kiungo machachari ndani ya uwanja Shiza Kichuya maarufu kama Kichuya kona, Hassani Dilunga, beki kisiki Pascal Serge Wawa raia wa Ivory Coast.

 Yusuph Mlipili beki mzawa wa kati ambaye maisha yake msimu huu yamekuwa ya tabu kikosi cha kwanza, Sharaff Eldin Shiboub kiungo raia wa Sudan.

Marcel Kaheza anayekipiga Polisi Tanzania kwa mkopo, Mohamed Rashid yeye yupo zake JKT Tanzania, Mohamed Ibrahim,'Mo Ibra' anayekipiga Namungo pamoja na Paul Bukaba ambaye yupo zake ndani ya Namungo.

KAGERA YAWAZA VPL


UONGOZI wa Kagera Sugar umesema kuwa umeukumbuka mpira baada ya kuukosa kwa muda mrefu kutokana na janga la Virusi vya Corona.
Machi 17, Serikali ilisimamisha shughuli zote za michezo kutokana na mlipuko wa Virusi vya Corona ambalo ni janga la dunia kwa sasa.
Akizungumza na Saleh Jembe, Kocha Mkuu wa Kagera Sugar, Mecky Maxime amesema kuwa miongoni mwa vitu ambavyo wamevikumbuka ni mpira ila hawana chaguo kwa kuwa afya ni jambo la msingi.
“Kiukweli kwa sasa tupo ila tumeukumbuka mpira na mashabiki ukizingatia kwamba ni muda mrefu umepita na hakuna ambacho kinaendelea ndani ya uwanja kwa sasa.
“Hatuna chaguo la kufanya kwa sasa kwa kuwa janga lililopo ni kubwa na kikubwa ni kuchukua tahadhari ili kuwa salama,” amesema Maxime.
Kagera Sugar ipo nafasi ya 8 ikiwa na pointi 41 baada ya kucheza mechi 10 kwenye ligi.

kumekucha huko chelsea


CHELSEA iliyo chini ya Kocha Mkuu Frank Lampard inapiga hesabu kupitisha panga la moto kwa wachezaji wake ili kujenga kikosi kipya msimu ujao.

Licha ya hali kuwa tete kiuchumi kutokana na janga la Virusi vya Corona ambavyo vimeivuruga dunia Chelsea inapiga hesabu ndefu za kushusha majembe mapya.

Miongoni mwa majina yanayotajwa sana ni pamoja na Jadon Sancho anayekipiga ndani ya Borussia Dortmund ambaye pia anawindwa na Manchester United.


Majina ya nyota ambao panga linawahusu ni pamoja na Tiemoue Bakayoko anayekipiga Monaco kwa mkopo, Marcos Alonso, Emerson Palmieri, Michy Batashuayi na David Zappacosta.